Ronaldo kwanini ameondoka?
IMEISHTUA dunia. Kwa nini Cristiano Ronaldo ameuzwa na Real Madrid kwenda Juventus? Mashabiki wa soka duniani kote wamepigwa na bumbuwazi baada ya staa wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo kuuzwa kwenda Juve kwa dau la Pauni 88 milioni juzi Jumatano mchana.
Guillem Balague, mchambuzi mahiri wa soka la Hispania amefichua siri kwa nini uhamisho wa staa huyo wa kimataifa wa Ureno kwenda Juventus umewezekana licha ya mashabiki wa soka kudhani isingewezekana.
Balague anaamini Ronaldo alikuwa anajihisi hatakiwi tena Santiago Bernabeu licha ya kucheza kwa misimu tisa yenye mafanikio huku akichukua taji lake la nne la Ulaya na wababe hao wiki chache zilizopita. Uhusiano wake na Rais, Florentino Perez ulidorora.
“Ni suala binafsi. Juventus ipo tayari kumlipa kiasi cha Euro 30 milioni kwa mwaka. Angeingiza kiasi hicho hicho cha pesa kama angesaini mkataba mpya na Real Madrid lakini aliona kama hatakiwi tena Madrid,” alisema Balague.
“Tatizo lilianzia mwaka mmoja uliopita, Perez alisema angemuongezea Ronaldo mshahara. Cristiano alikuwa anasubiria ofa na wakati huohuo Messi akapata mkataba mpya ambao ulimuingizia Euro 41 milioni kamili kwa mwaka, Neymar Euro 35 milioni kamili kwa mwaka, yeye alikuwa anaingiza Euro 21 milioni kwa mwaka.”
“Lakini pia anaona kuna mazungumzo makubwa kuhusu Neymar. Wakati Cristiano alipotwaa Ballon d’Or, Perez alisema kama Neymar anataka kutwaa tuzo hiyo, basi ahamie Real Madrid. Ronaldo hakupenda lakini hata alipotishia kuondoka Madrid wala haikujaribu kumshawishi abakie,” anaongeza Balague.
“Ilichanganya sana. Alikuwa anataka kuondoka lakini wakati huohuo alikuwa anataka aombwe kubakia. Madrid ilikuwa na furaha ya kumruhusu aondoke. Ilikuwa inataka aseme mwenyewe hadharani kwamba anaondoka ili lawama ziende kwake na sio kwao halafu baada ya hapo wangemuaga vema sana.”
Balague anaamini dau zima la Ronaldo kuanzia mauzo yake, thamani yake ya mkataba wa miaka minne linaweza kufika kiasi cha Euro 400 milioni na Juventus lazima iwe makini isibanwe na kanuni za matumizi sahihi ya pesa za Uefa.
“Ni wazi kanuni za pesa zitafanya kazi pale, hii ina maana inabidi iwe makini sana. Hata hivyo Madrid inaamini Juventus tayari imeshajua namna ya kulitatua hilo. Naamini ndani ya saa chache thamani ya Juventus katika soko la hisa itakuwa imepanda kwa kumchukua Ronaldo.” Kwa sasa Juventus inalazimika kuuza baadhi ya mastaa wake kwa ajili ya kummudu Ronaldo. Mmoja kati ya mastaa ambao wamekuwa wakihusishwa kuuzwa na Juventus ni pamoja na mshambuliaji wa kimataifa wa Argentina, Gonzalo Higuian ambaye ameripotiwa kutakiwa na Chelsea.
Mwingine ni mshambuliaji, Paulo Dybala ambaye ameanza kunyatiwa na klabu mbalimbali zikiwemo za England kama Liverpool na thamani yake inakadiriwa kuwa kubwa zaidi kuliko ya Muargentina mwenzake Higuain.
United zimemkosa vipi?
Kwa mujibu wa wakala wa Ronaldo, Jorge Mendes imeonyesha klabu nyingine mbili ambazo zilikuwa zinatajwa kumwania Ronaldo za PSG na Manchester Uniteds hazikuonyesha nia ya kumchukua na hivyo Juve kutimiza nia yake kiulaini.
Kwa kutua Juventus, Ronaldo ana uhakika wa kuongeza mataji katika kabati lake ambalo limejaa mataji tangu akiwa Manchester United.
Juventus imekuwa ikitawala soka la Italia kwa nguvu kubwa na kwa sasa imetwaa mataji saba mfululizo ya Ligi kuu ya Italia. Katika michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya bado haipo mbali sana ingawa mara ya mwisho ilichukua taji hilo msimu wa 1995/96.
Imefika fainali mbili katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Huku ikiwa na Ronaldo nafasi yake ya kwenda mbali zaidi huenda itakuwa inaimarika.
Comments
Post a Comment